Mtunzi:YOUNG NDABA DE LILIAN
Kulikuwa na usiku wa baridi katika kijiji cha Kinundu, kilichozungukwa na misitu minene na milima mirefu iliyoficha siri nyingi. Kijiji hicho kilijulikana kwa amani yake, lakini pia kwa matukio ya ajabu ambayo yalisimuliwa kizazi baada ya kizazi. Usiku huu haukuwa tofauti, anga lilikuwa giza totoro, na upepo ulivuma kama unabeba ujumbe wa hatari.
Katika kona ya mgahawa mdogo uliopewa jina Nyota ya Mwisho, Zuwena alikaa akitafakari maisha yake. Zuwena alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka ishirini na tano, aliyekuwa akijaribu kuishi maisha mapya baada ya kuvunjika moyo mara kadhaa. Alikuwa mchunguzi wa kujitegemea, anayejulikana kwa kufichua mambo ambayo watu walitaka kuficha. Siku mbili zilizopita, alipokea barua ya ajabu kutoka kwa mtu asiyejulikana, akimwomba kuchunguza kifo cha mwanamume aliyekuwa maarufu kijijini humo.
Ghafla, mlango wa mgahawa ulifunguliwa kwa kishindo, na baridi kali ikaingia. Mwanamume mwenye mwonekano wa kuvutia lakini wa kutisha alisimama mlangoni. Alikuwa amevaa koti nene la ngozi, na macho yake meusi kama mkaa yalionekana kana kwamba yanaweza kusoma mawazo ya mtu. Mwanamume huyo alitembea moja kwa moja hadi kwa Zuwena na kuketi bila kualikwa.
“Unaitwa nani?” aliuliza kwa sauti ya upole lakini yenye mamlaka.
Zuwena, akiwa amechanganyikiwa na uthubutu wake, alimtazama kwa makini. "Hili si swali ambalo mtu wa kawaida huuliza. Na wewe ni nani?" aliuliza kwa tahadhari.
Mwanaume huyo alitabasamu kwa upole lakini wa kutatanisha. “Mimi ni Yusufu, na si mtu wa kawaida.”
Kabla Zuwena hajapata muda wa kumjibu, kelele kubwa za mlipuko zilivuma kutoka msituni karibu na mgahawa. Watu waliokuwa ndani walikimbia kwa hofu, lakini Yusufu alibaki ameketi, mtulivu kama mawe. Alimtazama Zuwena kwa macho makali na kusema, “Najua kwa nini uko hapa. Na najua hiki ni mwanzo tu wa tatizo kubwa.”
Zuwena alisimama kwa haraka na kukimbilia nje. Alipofika, alikuta kijana aliyekuwa amelala chini, akiwa amejeruhiwa vibaya. Uso wake ulikuwa umejaa damu, lakini macho yake yalikuwa yameelekeza kwa Zuwena kana kwamba alikuwa na ujumbe wa haraka.
“Huyu ni nani?” Yusufu aliuliza, akiwa amesimama nyuma yake kimya kama kivuli.
Zuwena alihisi baridi ikipita mgongoni mwake. Mtu aliyelala pale alikuwa kijana aliyemkabidhi barua ya siri siku mbili zilizopita, na sasa alikuwa nusu mfu. Kabla hajapata nafasi ya kujibu, Yusufu alimchukua mkono na kusema kwa sauti ya kuamuru, “Kama unataka kuishi na kufahamu ukweli, utahitaji kuniamini. Muda unayoyoma.”
Mwisho wa Sehemu ya Kwanza

Maoni